Wananchi wa Katumba Azimio wafurahia Zahanati


Wananchi wa kijiji cha Katumba Azimio, kata ya Pito wameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwa kuwajengea Zahanati inayotarajiwa kutoa huduma kwa kijiji hicho na vijiji vya jirani vyenye jumla ya kaya 1,099.

Zahanati ya Katumba Azimio

Ujenzi huo wa zahanati uliomalizika mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu umegharimu shilingi 130,176,000 huku serikali kuu ikiwa imechangia shilingi 53,500,000, wananchi nao wakiwa wamechangia shilingi 25,850,000 na manispaa ikiwa imechangia 50,826,000.

Mmoja wa Wananchi wa kijiji cha katumba Azimio Herman Maufi amesifu kasi ya serikali ya awamu ya tano katika kuhakikisha sekta ya afya inaimarika kuanzia ngazi ya kijiji haji wilaya “Sisi tunamshukuru Mkurugenzi wetu wa Manispaa kwa kuona umuhimu wa kutusogezea huduma hii karibu lakini Zaidi sifa hizi zimfikie rais wetu jemedari Dkt. John Pombe magufuli kwakweli anapiga kazi.”

Nae mwananchi mwingine wa kijiji cha jirani Tausi Juma amesema kuwa uwepo wa zahanati hiyo unawasaidia kuepuka kwenda mjini kupata huduma hiyo na matokeo yake watoto wao watapata huduma iliyokaribu nao na hatimae kuepuka gharama za kwenda mbali kufuata huduma hiyo.

Comments