Wananchi 8000 kufaidika na Mradi wa maji Kasense-Chipu


Zaidi ya wananchi 8000 wa vijiji vya Kasense na Chipu katika Manispaa ya Sumbawanga wameondokana na kero ya muda ya mrefu ya ukosefu wa maji ya salama ya kunywa baada ya kujengewa mradi wa maji bomba la mserereko unaohudumia wa vijiji hivyo.
Maji
Mradi huo wa maji ambao tanki lake limejengwa kwenye kijiji cha Kasense umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 782.1 ikiwa ni fedha kutoka serikali kuu, huku halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ikichangia Shilingi Milioni tatu na wananchi wa vijiji hivyo wakichangia nguvu zao kwa thamani ya Shilingi Laki Tisa na hamsini Elfu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Hamid Njovu alisema kukamilika kwa mradi huo kutawafanya wananchi hao kuepukana na magonjwa ya homa za matumbo, kuhara na kipindupindu, kutokana na kupata maji safi na salama, tofauti na awali walipokuwa wakitegemea kuteka maji kwenye visima vya kienyeji.
Njovu alisema mradi huo ulianza kutekelezwa kuanzia mwezi  Mei mwaka uliopita na kukamilika mwezi Machi 2018.
Mhandisi wa maji wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Kazoya Mong’ateko alisema mradi huo wa maji unajumuisha vituo vya kuchotea maji (DPs) 33 katika umbali usiozidi mita 400 na hivyo kuokoa muda wa wananchi waliokuwa wakitumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji safi na salama.
Mhandisi wa maji katika Manispaa ya Sumbawanga Mhandisi Kazoya Mong’ateko amesema ongezeko la wananchi wanaotumia maji limeongezeka kutoka asilimia 50 hadi 60.
Mhandishi Mong’ateko alisema kukamilika kwa mradi huo kunazidi idadi ya vituo vya vya kutekea maji vilivyo karibu na wananchi tofauti na vituo 64 vilivyokuwapo hapo awali hadi sasa ambapo kuna vituo 424, na kuongeza kuwa hiyo ni hatua kubwa ya mafanikio kwa halmashauri yake.
Alisema hivi karibuni Manispaa ya Sumbawanga imekamilisha na miradi ya maji ya mwaka 2017/18 katika mtandao wa bomba kwenye vijiji vya Kasense, Chipu, Matanga na Kisumba ambapo katika miradi hiyo jumla ya Lita 315,000 zinapatakana kila siku, huku ikifanikiwa kujenga tanki kubwa la maji katika eneo la Mtipe ambalo linakusanya maji kutoka chanzo cha Salumbwa- Chelenganya-Mtipe.

Comments