ALAT Rukwa waishauri Wizara ya Maji kutumia wataalamu wa maji wa halmashauri kusanifu wa miradi ya maji.


Wajumbe wa mkutano wa ALAT mkoa wa Rukwa wameishauri Wizara ya Maji kutuwatumia wataalamu wa Halmashauri husika katika kusanifu miradi ya maji kwenye halmashauri zao ili kuondoa uwezekano wa miradi mingi kushindwa kufanikiwa katika utekelezaji wake.
Maji
Akizungumza katika kikao kilichofanyika mjini Matai wilayani Kalambo, Mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Rukwa  Mh.Kalolo Ntila alisema hoja nyingi zinazotokea katika miradi ya maji zimekuwa zikichangiwa na sababu nyingi na moja wapo ikiwa ni usanifu wa miradi ya maji unaofanywa na Wataalamu toka nje  ya halmashauri zao usiozingatia hali halisi ya mazingira na vigezo vya maeneo husika .
Mh.Ntila alisema kumekuwa na changamoto nyingi zinazotokea katika utekelezaji wa miradi hiyo baada ya ujenzi wake maji kushindwa kuwafikia wananchi au kufika kwa kiwango cha chini kutokana aidha mradi kujengwa kwenye vyanzo vya maji visivyo na uhakika au sababu zinginezo za kimazingira.
“Wataalamu wa halmashauri na wananchi wa maeneo yetu wanayafahamu vyema mazingira yao, hivyo ipo haja ya wataalamu wanaotoka nje ya halmashauri kuwashirikisha kabla ya mradi kuanza kujengwa ili nao watoe ushauri wao na kuepukana na changamoto zinazoweza kutokea hapo baadaye”.alisema Ntila
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga Mh.Jastin Malisawa alisema kuwa Wataalamu wa maji wa halmashauri wana weledi wa kutosha katika utendaji wa kazi zao kama walivyo wale kutoka Wizara ya maji hivyo hakuna sababu ya kuwatenga katika usanifu wa miradi ya maji kwakuwa hata vyuo walivyosoma ni vya aina moja.
Mh.Mwanisawa alisema Wataalamu wote ni watumishi wa serikali hivyo ingelipendeza iwapo kila mtu akashiriki katika kutoa ushauri wake ili Taifa liweze kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kwa kasi zaidi pasipo kupata vikwazo vya miradi yake kutekelezwa katika kiwango kisichoridhisha, hali inayochangia kuongeza kwa fedha katika kubadili mifumo ya usanifu wa miradi hiyo au gharama za nyongeza za kuwalipa wakandarasi.
Katika tathimini ya kikao hicho kuhusu miradi ya maji Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ilionekana kufanya vizuri zaidi, ikifuatiwa na halmashauri ya wilaya ya Kalambo, wakati halmashauri ya wilaya ya Nkasi ikionekana kuwa na changamoto nyingi katika miradi yake.


Comments