Wafanyabiashara wakubwa wa mbolea Mkoani Rukwa pamoja na
wakulima wameridhishwa na upatikanaji wa mbolea na kusifu juhudi za serikali
baada ya kupaza sauti zao na kusikika na Rais Dk. John Pombe Magufuli na jambo
hilo kufanyiwa kazi ndani ya muda mfupi.
Wafanyabiashara hao wamesema kuwa wakulima hivi sasa
hawapangi tena foleni kusubiri mbolea iliyokuwa ikipatikana kwa taabu na kwa
kunyang’anyiana na kuwa foleni hizo zimekwisha na wakulima hawana haja ya
kutoka Kijiji kuja mjini kufuata mbolea kwani mbolea hizo zinawafuata huko
waliko hasa baada ya marekebisho ya bei elekezi iliyotolewa na Uongozi wa mkoa
wa Rukwa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.
Mmoja wa Wafanyabiashara hao wakubwa Mohamed Rashid Mdangwa
wa Kampuni ya ETG amesema “Sasa wakulima wameanza kupata mbolea kwa wingi,
mwanzo walikuwa wanapanga foleni hapa lakini kuanzia ile Jumatatu agizo la Rais
kuwa mbolea iende Mkoa wa Rukwa, sasa hivi population (wingi) ya watu imepungua
sana, sasa hivi mahitaji ya mbolea sio
makubwa sana kama miezi miwili iliyopita,na mbolea ipo nyingi njiani inakuja,
na bei elekezi aliyoitoa Mkuu wa Mkoa imesaidia mbolea kufika vijijini kupitia
wakala wadogo wa mbolea.”
Yamewsemwa hayo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kupitia maghala
makubwa ya mbolea yaliyopo Sumbawanga Mjini pamoja na baadhi ya wasambazaji
wadogo ili kujionea upatikanaji wa mbolea hizo tangu kutolewa kwa agizo la Rais
Dk. John Pombe Magufuli la kusambaza mbolea hizo katika Mikoa inayoongoza kwa
uzalishaji wa chakula nchini tarehe 8.1.2018.
Mh. Wangabo aliwasihi wasambazaji wadogo wa mbolea kuendelea
kujitokeza na kununua mbolea hiyo ambayo bei iliyopo sasa imezingatia maoni yao
na haiumizi, hivyo kufanya hima kuhakikisha kuwa mkulima hakosi mbolea ili
kuweza kubaki katika lengo la kuzalisha chakula kwa wingi na kuleta ushindani
na mikoa mingine inayozalisha chakula.
“Mimi nitoe wito tu kwa wale Agrodealers (wasambazaji wadogo
wa mbolea) wafike kuendelea kununua mbolea, hata bei tumekwishazifikiria tena
upya, kila Halmashauri katika Wilaya wamekwisha kaa na kutoa mapendekezo yao
halisi ya kiusafirishaji, kwahiyo wafike wanunue mbolea na kutakuwa na faida,
bei imezingatia hadi miundombinu iliyoharibika hakutakuwa na usumbufu,” Mh.
Wangabo alifafanua.
Mh. Wangabo alitembelea maghala matatu ya wafanyabiashara
wakubwa waliopo mjini sumbawanga, TFC pamoja na maduka ya wasambazaji wadogo matatu
na kuongea na baadhi ya wakulima ili kujithibitishia upatikanaji wa mbolea hiyo
kwa maeneo ya mjini na inayopelekwa vijijini.
Kwa msimu wa 2016/2017 Mkoa
wa Rukwa ulilima Hekta zipatazo 556,975.9 na kuvuna tani 1,109,055.6 za mazao
ya chakula kati ya hizo mahindi yalikuwa tani 710,602. Kwa msimu huu wa Kilimo
wa 2017/18 Mkoa umelenga kulima jumla ya eneo la Hekta 554,310.6 na kuvuna tani
1,669,746.2 za mazao ya chakula.
![]() |
Mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa, Kamanda wa Zimamoto Mkoani Rukwa akikagua mbolea katika ghala la Kampuni ya Mbolea ya Taifa (TFC) lililopo Sumbawanga Mjini. |
![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili kutoka kulia) akiwa amesimama mbele ya duka la mbolea kuulizia upatikanaji wa bidhaa hiyo katikati ya mji wa sumbawanga, Mkoani Rukwa. |
Comments
Post a Comment