TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
*Ni la MSD litahudumia
mikoa mitatu ya kanda ya Tabora
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua duka la dawa la Bohari Kuu
ya Dawa (MSD) katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda lilogharimu sh. milioni 55
litakalohudumia mikoa mitatu ya Kigoma, Katavi na Tabora.
Pia duka hilo itatoa huduma kwa vituo vya kutolea huduma za afya
580 ikiwa ni pamoja na hospitali za rufaa za mikoa miwili ya Kigoma na Tabora,
Hospitali za wilaya sita za Nzega, Igunga, Urambo, Kobondo, Kasulu na Mpanda
Mji.
Waziri Mkuu amefungua duka hilo la dawa la MSD,
lililoko katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi leo
(Jumanne, Januari 17, 2017) ikiwa ni utekelezaji wa agizo
alilolitoa kwa MSD Agosti 20, 2016 alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani
Katavi. Aliuagiuza uongozi MSD kujenga duka hilo ili kurahisisha
upatikanaji wa dawa katika mkoa huo pamoja na mikoa jirani.
Aidha, Waziri Mkuu amesema baada ya kufunguliwa kwa duka hilo
Serikali haitarajii kusikia tena katika vituo vya afya na Zahanati zilizoko
mkoani Katavi na mikoa jirani zinakosa dawa. Amewaagiza Wakurugenzi
kusimamia suala hilo na kuhakikisha vituo vyote vya afya vinakuwa na dawa za
kutosha.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia Wazee na Watoto kukutana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) ili kutafuta namna bora ya kutumia fedha za huduma za afya
zinazipatikana katika halmashauri nchini.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 kwa
ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Katavi ili kupunguza msongamano
wa wagonjwa katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda.
Amesema lengo la Serikali ni kuwa na Hospitali ya Rufaa kwa kila
mkoa, hivyo, Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa mipya itakayojengwa Hospitali
ya Mkoa ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Laurean Bwanakunu
amesema ujenzi waduka hilo la Mpanda hadi kukamilika umegharimu sh. milioni 55,
huku benki ya CRDB ikitoa sh. milioni 50 na MSD imeweka dawa na vifaa tiba vya
sh. milioni 104.45 na vifaa vya TEHAMA vya sh. milioni tano.
Amesema kuanzishwa kwa duka hilo kutaongeza upatikanaji wa dawa
na vifaa tiba kwa wagonjwa hasa dawa ambazo hazimo katika orodha
zilizoidhinishwa na Serikali kutumika katika vituo vyake vya kutolea huduma za
afya ila zimeidhinishwa kutumika nchini na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Amesema dawa na vifaa tiba vilivyomo katika orodha ya Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) zinapatikana katika duka hilo kwa bei nafuu, hivyo
kuondoa usumbufu kwa wagonjwa kwenda kuzitafuta katika maduka ya mbali na kwa
bei ghali.
“Nitoe mfano mdogo wa tofauti ya dawa katika ya maduka ya MSD na
maduka ya mitaani, hapa dawa ya sindano ya kutibu fungus aina ya Fluconazole
inauzwa sh. 2,300 na mitaani sh. 4,500 na dawa ya sindano kwa ajili ya kushusha
kisukari (Insulin) chupa moja MSD ni sh. 8,500 na mitaani sh. 20,000,” amesema.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, JANUARI 17, 2017.
Comments
Post a Comment