WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema jumla ya vijiji 53 vya mkoa wa Njombe vitapatiwa huduma ya
maji safi na salama katika mwaka huu wa fedha.
Alitoa kauli hiyo jana
(Jumamosi, Januari 21, 2017) wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya
Wanging’ombe katika mkutano wa hadhara katika kata ya Ilembula.
Waziri Mkuu alisema
zaidi ya sh. bilioni 2.4 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia mradi huo wa maji
katika miji ya Makambako, Njombe na wilaya ya Wanging’ombe.
Alisema kati ya vijiji
hivyo vitakavyopatiwa maji, vijiji 22 ni vya wilaya ya Wanging’ombe, hivyo
aliwaomba wananchi hao kuwa na subira.
Kwa mujibu wa Waziri
Mkuu tayari zabuni ya mradi huo imeshatangazwa, hivyo amewaagiza viongozi wa
Wizara ya Maji na Umwagiliaji watafute mkandarasi mzuri.
Alisema lengo la
Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji
katika umbali usiozidi mita 400 kutoka mahali anapoishi.
Waziri Mkuu alitoa
kauli hiyo baada ya Mbunge wa Wanging’ombe, Mheshimiwa Mhandisi Gerson Lwenge
kumuomba awasaidie katika kutatua kero ya maji.
Mbunge huyo ambaye pia
ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji alisema “Mheshimiwa Waziri Mkuu sisi
tunakabiliwa na changamoto ya maji, leo tunaomba ututatulie kero hii”.
Changamoto nyingine
aliyoitaja Mheshimiwa Lwenge ni pamoja na ukosefu wa hospitali ya wilaya,
ambapo Waziri Mkuu aliigiza halmashauri hiyo kuanza ujenzi.
Alisema Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 inaelekeza kuwa na hospitali katika kila
wilaya, kituo cha afya kwa kila kata na zahanati kwa kila kijiji.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya
hiyo Bw. Ally Kasinge kukutana na viongozi wa kata na vijiji vinavyozunguka
hifadhi ya Mapanga Kipengele ili kutatua kero ya mpaka.
(Mwisho)
Comments
Post a Comment