Mkurugenzi Manispaa ya Sumbawanga aipongeza REYO


Mkurugenzi wa manispaa ya Sumbawanga Hamid Njovu ameipongeza taasisi ya vijana inayojishughulisha na mazingira Rukwa Environmental Youth Organization (REYO) katika kuwahamasisha wananchi kupanda miti ili kutunza mazingira ya manispaa.

Kitalu cha miti REYO

Amesema kuwa ili kuendelea kutunza hali ya hewa safi iliyopo katika mji wa Sumbawanga kila mmoja ana nafasi ya kuhakikisha tunafanikiwa kupanda miti mingi iwezekanavyo kwakuwa miti inafaida nyingi ikiwemo matunda kwaajili ya kuboresha afya, mbao ambazo huitajika kutengeneza samani ambazo huongeza ajira nchini.

“Nichukue nafasi hii kukipongeza kikundi cha REYO, wanatusaidia katika kuhakikisha tunafikia malengo ya kupanda miti milioni 1.5 katika mwaka wa fedha 2017/2018 ambayo ni malengo ya kimkoa ambapo wao hadi sasa wamegawa bure miche 16,870 katika tasisi za serikali na kuotesha miche 135, 000,” Amesema.

Ameongeza kuwa kikundi hicho kimefanikiwa kutoa ajira kwa vijana 23 Kutoa mafunzo ya uanzishwaji wa vitalu kwa vitendo kwa vijana 18 ambao wamejiajiri na wanaendelea na kazi hii katika mkoa wa Rukwa na Katavi.

Katika mwaka wa fedha 2017/2018 maandalizi ya upandaji miti yanaendelea ambapo mpaka sasa Manispaa ya Sumbawanga ina jumla ya vitalu 24 vya miti vilivyoanzishwa ambavyo vina zaidi ya miche 980,000 ya matunda na mbao.

Comments