Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ipo mbioni kukamilisha
miradi ya maji inayofadhiliwa na benki ya Dunia kwa kushirikiana na serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia programu ya maji na usafi wa mazingira
vijijini (NRWSSP) ili kukata kiu ya wananchi katika kupambana na shida ya maji.
Haya ni kutokana na azma ya serikali ya kuongeza upatikanaji
wa huduma ya maji safi na salama kufikia asilimia 72 vijijini na asilimia 95
mijini hadi ifikapo mwaka 2025.
![]() |
Mwananchi akichota maji kijiji cha Malonje - Sumbawanga |
“Kwa sasa katika Manispaa
ya Sumbawanga, vijijini vilivyofikiwa na huduma ya maji ni asilimia 49.9 na
mjini ni asilimia 62.” Mhandisi wa maji wa Manispaa Bi. Kazoya alisema.
Miradi hiyo inalenga kuhusisha vijiji vya Mlanda, Pito,
Malagano, Tamasenga, Malonje, Kisumba, Matanga, Kasense, Chipu, Mponda,
Mawenzusi, Katumba Azimio, Nambogo, Chelenganya, Luwa, Kanondo na Milanzi.
Miradi mitano inayohusisha vijiji vya Kanondo, Mlanda, Pito,
Malagano, Tamasenga na Malonje inaelekea kukamilika na inatarajiwa kuhudumia wananchi
40,492 kwa miaka kumi ijayo.
Akitoa mfano wa mradi unaotarajia kuisha, Afisa wa maji wa
Manispaa ndugu John Mlwafu alisema “mradi huu wa Pito, Malagano na Tamasenga unajegwa
na Mkandarasi Girison Investment Co. Ltd kwa gharama ya shilingi Milioni 532
bila VAT, na mpaka sasa mradi huu umefikia asilimia 80 ya matengenezo.”
![]() |
Afisa wa Maji, John Mlwafu akifafanua Mradi kwa wafanyanyazi wenzake. |
Mlwafu aliongeza kuwa mradi huo ulitakiwa kuisha tangu
Februari 02 mwaka huu, lakini kutokana na changamoto zilizo nje ya uwezo jambo
hilo halikuweza kukamilika.
“Mvua nyingi zilizonyesha ziliathiri kwa kiwango kikubwa
sana kasi ya ujenzi wa miradi, lakini pia wakandarasi kuwa na miradi mingi
kuliko uwezo wao,” Mlwafu alisisitiza.
![]() |
Tanki la Maji Malonje |
Katika kujiletea maendeleo vijijini na mijini, jamii inapaswa
kuchangia asilimia 2.5 ya gharama za miradi ili nao waweze kuilinda na kuitunza
na kuifanya ni ya kwao kwa faida yao.
Comments
Post a Comment