Kituo cha Afya Mazwi chaboreshwa ili kuhudumia wananchi 94,856


Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imeendelea na ujenzi wa upanuzi wa kituo cha afya Mazwi kilichopatiwa shilingi milioni 500 na serikali kuu ili kuboresha huduma za afya na kutarajiwa kuhudumia wananchi 94,856.

Kituo cha Afya Mazwi

Kituo hicho kinachoendelea na ujenzi kimeongeza majengo ya Maabara, Kichomea taka, Jengo la Mama Baba na Mtoto, Vyoo na Kibanda cha mlinzi tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya azma ya serikali kuboresha kituo hicho.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Sumbawanga Dkt. Archie Hellar ameishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutenga fedha hizo na kuweza kuboresha huduma ya afya katika manispaa ya Sumbawanga yenye kituo kimoja cha afya kinachomilikiwa na serikali.

“Kuimarisha huduma za Afya kwa wananchi kwa kusogeza huduma  karibu kwa zaidi ya Wakazi 94,856 wa Kata ya Mazwi na maeneo mengine yasiyo za Zahanati wala kituo cha afya ikiwemo Kata za Izia, Momoka , Mafulala, Msua ,Lwiche  na Sumbawanga asilia,” Amesema.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kutawezesha kupunguza vifo vya mama na mtoto, kuwezesha watoto wote kupata chanjo kwa wakati ili kuwakinga na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo, pamoja na kuijenga jamii iliyo na watu wenye Afya nzuri  na kushiriki katika shughuli mbalimbali za Maendeleo.

Kwa sasa Halmashauri ina jumla ya vituo vya tiba 42 ikiwemo Hospitali 2 ya rufaa ya Mkoa na DDH, Vituo vya Afya 3 kimoja kikiwa cha serikali, na zahanati 35, 20 zikiwa za serikali.

Comments